Kikosi chetu leo saa nne usiku kwa saa za Morocco kitashuka katika Uwanja wa Mohamed wa tano kuikabili Raja Casablanca katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tunaingia kwenye mchezo huu tukiwa wote tumefuzu hatua ya robo fainali kutoka katika kundi C.
Kocha mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ ameweka wazi kuwa ingawa matokeo yoyote ya mchezo hayataathiri msimamo wa kundi lakini tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri.
Robertinho amesema malengo yetu kwenye mchezo wa leo ni kuhakikisha tunacheza vizuri na kupata matokeo ya ushindi.
“Haitakuwa mechi rahisi, Raja ni timu nzuri lakini Simba ni timu kubwa na tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri,” amesema Robertinho.
Taarifa ya Kikosi….
Wachezaji wapo kwenye hali nzuri, wamefanya mazoezi ya mwisho usiku wa kuamkia leo na wapo kamili kwa mchezo.
Nyota wote wa Kimataifa ambao walikuwa kwenye majukumu ya timu za taifa wao wamewahi kufika kabla ya msafara wa timu uliotoka jijini Dar es Salaam.
Walitufunga kwa Mkapa…..
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Februari 18 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa tulipoteza kwa mabao 3-0.
Zimbwe Jr kuikosa Raja……
Mlinzi wa kushoto Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ ataukosa mchezo wa leo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano.