Preview: Mchezo wetu dhidi ya Singida Big Stars

Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ leo atakiongoza kikosi chetu kuikabili Singida Big Stars katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku.

Mchezo uliopita wa Kombe la FA dhidi ya Coastal Union kikosi kilikuwa chini ya kocha msaidizi, Juma Mgunda kutokana na Robertinho kuwa nchini kwao Brazil kushughulikia masuala ya kifamilia.

Mchezo wa leo utakuwa watatu wa Robertinho kukiongoza kikosi chetu baada mechi dhidi ya Mbeya City tuliobuka na ushindi wa mabao 3-2 na ule wa ugenini dhidi ya Dodoma Jiji tulioshinda 1-0.

Hali ya Kikosi

Kikosi kipo kwenye hali nzuri na wachezaji wote wamefanya mazoezi kujiandaa na mtanange wa leo ambao tunaamini utakuwa mgumu.

Mlinzi wa kati Henock Inonga na winga Peter Banda ambao walikuwa majeruhi wapo fiti na benchi la ufundi likiona inafaa linaweza kuwatumia katika mchezo wa leo.

Mshambuliaji Moses Phiri ambaye licha ya kufanya mazoezi ya pamoja na wenzake hatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kutokana na kuendelea kutengeneza utimamu wa mwili.

Mgunda aiwahi Singida

Kocha Msaidizi, Juma Mgunda ambaye alisafiri kuelekea nyumbani kwao Tanga kwa ajili ya kumuuguza mama yake amerejea jana mchana na amejiunga na benchi la ufundi kuongoza kikosi katika mchezo wa leo.

Baada ya kurejea moja kwa moja Mgunda aliungana na kikosi na alikuwepo kwenye mazoezi ya mwisho jana jioni katika Uwanja wa Mo Simba Arena.

Tulitoka sare mchezo wa kwanza

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa katika Uwanja wa Liti uliopigwa Novemba 9 ulimalizika kwa sare ya kufungana bao moja.

Wenyeji Singida walipata bao lao kupitia kwa Deus Kaseke wakati sisi tulisawazisha kupitia kwa Peter Banda.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER