Kocha Mkuu Pablo Franco, amefunguka kuwa anatarajia mashabiki watajitokeza kwa wingi kumpa ukaribisho kwenye mchezo wake wa kwanza wa nyumbani ambao utakuwa wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia utakaopigwa Benjamin Mkapa Jumapili.
Pablo amesema katika mchezo wa kwanza kuingoza timu ambao ulikuwa wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting Ijumaa iliyopita mashabiki walijitokeza kwa wingi Uwanja wa CCM Kirumba hatua iliyompa faraja.
Pablo raia wa Hispania ameongeza kuwa anaamini Jumapili mashabiki watakuwa wengi zaidi kwenye dimba la Benjamin Mkapa kuliko ilivyokuwa Kirumba wiki iliyopita ili kumpa ukaribisho.
“Nawashukuru sana mashabiki waliojitokeza kwa wingi sana kule Mwanza, naamini watakuja kunikaribisha kwa wingi Jumapili wakiwa na jezi nyekundu uwanja mzima,” amesema Kocha Pablo.
Akizungumzia mchezo wenyewe dhidi ya Red Arrows, Pablo amesema utakuwa mgumu na tunapaswa kucheza kwa kujitoa asilimia 100 katika muda wote wa dakika 90 ili kupata ushindi nyumbani.
“Mechi itakuwa ngumu, tupo nyumbani inatupasa kujituma kwa asilimia 100 muda wote wa mchezo ili tupate ushindi. Maandalizi yanaendelea vizuri na matarajio yetu ni kupata ushindi,” amesema Pablo.
One Response