Hakuna lugha rahisi ambayo unaweza kuitumia kuelezea jinsi ambavyo tunahitaji ushindi mnono kwenye mchezo wetu wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini utakaopigwa leo Uwanja wa Amaan Zanzibar saa 10 jioni.
Tunahitaji kushinda kwa idadi kubwa ya mabao ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufanya vema katika mechi ya marudiano itakayopigwa Jumapili ijayo nchini Afrika Kusini ndio maana ya ‘Ama zetu ama zao’.
Kwa kifupi mpaka hapa tulipofikia hakuna jambo jingine tunalotaka zaidi ya kutinga fainali na hatimaye kutwaa taji la michuano hii ya pili kwa ukubwa Afrika.
Bodi ya Wakurugenzi, Menejimeti, Benchi la ufundi, wachezaji, wanachama mpaka mashabiki wanaimba lugha moja tu nayo ni kuiona timu ikitwaa ubingwa wa michuano hii mwishoni mwa msimu.
Fadlu asisitiza umakini kwa wachezaji
Kocha Mkuu, Fadlu Davids amewataka wachezaji kuwa makini na kuondoa makosa madogo madogo ambayo yanaweza kuwapa faida wapinzani wetu na ikiwezekana tupate ushindi bila kuruhusu bao ili tukienda Afrika Kusini tukamalize mechi.
“Hatupaswi kufanya makosa ambayo yanaweza kutugharimu, tunahitaji kutumia vizuri uwanja wa nyumbani ili tukienda ugenini iwe rahisi kumalizia,” amesema Fadlu.
Che Malone atoa somo kwa washambuliaji
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kati, Che Fondoh Malone amesema wanafahamu hatua tuliyopo inaamuliwa na mtaji wa mabao kitu ambacho wamepanga kukifanya kwa asilimia 100 huku pia wakihakikisha haturusu nyavu zetu kuguswa.
“Tutaingia kwa kucheza mpira tuliouzoea, hatutakuwa na presha lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi wa mabao mengi katika uwanja wa nyumbani na hilo litawezekana kama mashabiki watakuja kwa wingi kuja kutushangilia,” amesema Che Malone.
Hatujawahi kukutana na Stellenbosch kabla
Mchezo wa leo ni wa kwanza kukutana na Stellenbosch katika historia ya timu hizi na pia tunakutana katika ardhi ya Zanzibar ikiwa ni mara ya kwanza kwetu kucheza mechi ya nusu fainali Visiwani humo.