Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ambaye ni Rais wa Klabu, Mohamed Dewji ‘Mo’ amewataka mashabiki na wapenzi wa timu yetu kuwa watulivu kipindi hiki wakati tunapoandaa kikosi cha msimu ujao.
Mo amesema mashabiki wanajisikia vibaya kutokana na jinsi tulivyomaliza msimu wa Ligi 2024/2025 lakini Uongozi unaendelea kuhakikisha tunakuwa na timu imara zaidi.
Mo amesema huu si wakati wa kubishana wala kumtafuta mchawi badala yake kuwa wamoja ili kuhakikisha tunakuwa imara kuelekea msimu mpya wa mashindano 2025/2026.
Aidha Mo ameweka wazi kuwa Simba haijaanguka bali inapitia kipindi cha mpito, msimu uliopita tumejenga kikosi kipya, tumeimarisha benchi la ufundi, tumeweka mwelekeo mpya ambao umefika hatua nzuri.
Mo ameenda mbali zaidi kwa kusema hata msimu uliopita haukuwa mbaya kwani tulifika zaidi ya matarajio tuliyokuwa tumejiwekea kama ambavyo tutafanya kwenye msimu mpya.
“Naomba tuendelee kuwa wavumilivu, tunaendelea kufanya marekebisho makubwa, tuendelee kusimama pamoja kama familia moja. Mbele kuna mwanga, na pamoja tutarudi tukiwa imara zaidi,” amesema Mo Dewji.