Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda amesema maandalizi ya mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC utakaopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid saa 10 jioni yamekamilika.
Mgunda amesema kikosi kipo kwenye hali kuelekea kwenye mtanange huo na tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa KMC.
Mgunda ameweka wazi kuwa katika mchezo wa kesho tutamkosa mshambuliaji Pa Omar Jobe ambaye alipata maumivu katika mchezo uliopita dhidi ya Geita pamoja na Kibu Denis aliyerejea kutoka majeruhi lakini bado hana utimamu wa mwili.
“Maandalizi ya mchezo yamekamilika, wachezaji wangu wapo kwenye hali nzuri tayari kwa ajili ya mechi ngumu dhidi ya KMC kesho.
“Jambo la kushukuru ni kwamba baadhi ya wachezaji wetu waliokuwa majeruhi Luis Miqussone na Clatous Chama wamepona na tumekuja nao kwa ajili ya mchezo wa kesho,” amesema Mgunda.
Akizungumza na mashabiki Mgunda amesema “Mimi ni muumini wa uwepo wa mashabiki uwanjani. Tunathamini sana mchango wao na tunawaomba waje kwa wingi kesho kwa ajili ya kuipa nguvu timu.”
Kwa upande wake mlinda mlango, Ally Salim amesema wachezaji wote wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo na lengo la kila mmoja ni kuhakikisha anaisaidia timu kupata matokeo chanya.
“Sisi kama wachezaji tupo tayari kwa mchezo, tunafahamu utakuwa mchezo mgumu. Tunaiheshimu KMC lakini tupo hapa kupambana hadi mwisho ili tupate pointi tatu,” amesema Ally Salim.