Kocha Mkuu Juma Mgunda, amesema kwenye mashindano yoyote hakuna timu ndogo ndiyo maana katika mchezo wa kesho wa hatua ya pili ya Azam Sports Federation Cup hatutwadharau wapinzani wetu Eagle FC.
Mgunda amesema michuano ikifikia hatua ya mtoano lolote linawezekana na hutakiwi kuonyesha dharau kwa timu yoyote bila kujali inashiriki ligi daraja la ngapi.
Mgunda amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika wachezaji wapo kwenye hali nzuri ambapo baada ya timu kurudi kutoka Tanga mazoezi yalianza mara moja kujiwinda na Eagle.
“Maandalizi ya mchezo wa kesho yamekamilika wachezaji wapo kwenye hali nzuri, tunaenda kukutana na timu ambayo haina jina kubwa lakini haya ni mashindano. Tumejiandaa vizuri na hatutaidharau Eagle,” amesema Mgunda.
Kuhusu hali ya kikosi Mgunda amesema tutawakosa Sadio Kanoute anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu, Joash Onyango, Israel Patrick na Peter Banda ambao ni majeruhi.
Kiungo Nelson Okwa amerejea kikosini na tayari ameanza mazoezi na wenzake hivyo anatarajia kumpa dakika za kucheza kwenye mchezo wa kesho.