Msanii wa Bongo Fleva, Mbosso amewapagawisha maelfu ya mashabiki wetu waliojitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye kilele cha Tamasha la Simba Day.
Mbosso ameziimba karibia nyimbo zake zote ambazo zimetamba kwa nyakati tofauti huku Pawa na Aviola zikionekana kupendwa zaidi.
Wakati akiendelea kutoa burudani Mbosso aliweka wazi kuwa kupata baraka kutoka Mwanamuziki Nguli, Ally Kiba ambaye ametumbuiza mara mbili kwenye Tamasha la Simba Day.
Mbosso amefunguka kuwa alikuwa na ndoto ya kutumbuiza kwenye kilele cha Simba Day na imetimia kitu ambacho kimemfurahisha huku akiweka wazi kuwa yeye ni Mwanasimba damu.
“Kaka yangu Ally Kiba amenipa baraka nyingi kuelekea siku hii ya leo kwakuwa mwenzangu ana uzoefu mkubwa na nimefurahi leo kutimiza ndoto ya kutumbuiza kwenye kilele cha Simba Day,” amesema Mbosso.