Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa Liti kuikabili Singida Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Wachezaji wamefanya mazoezi ya mwisho jana jioni na hakuna ambaye amepata maumivu yatakayomfanya kuukosa mchezo wa leo.
Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu na tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Singida lakini tumejipanga vizuri kuhakikisha tunashinda.
Robertinho kuwashushia Singida ‘fulu Mziki’,…….
Robertinho ameweka wazi kuwa anawaamini wachezaji wake wote lakini katika mchezo wa leo atawatumia wale wa kikosi cha kwanza kutokana na ugumu wa mchezo.
“Tunapaswa kucheza vizuri na kushinda kama kawaida. Tutatumia kikosi chetu cha kwanza kwakuwa ni mchezo mgumu lakini nawaamini wachezaji wangu wote,” amesema Robertinho.
Wachezaji wapo tayari kwa pambano….
Mlinzi wa kati, Kennedy Juma amesema dakika 90 za leo zitaamua nani ataondoka na pointi tatu ingawa kwa upande wao wachezaji wapo tayari kwa mchezo.
“Tupo tayari kwa mchezo, tunafahamu utakuwa mgumu Singida ni timu imara lakini nasi tumejiandaa vizuri na dakika 90 zitaamua,” amesema Kennedy.
Tulitoka sare mara ya mwisho Liti….
Mara ya mwisho tulivyokutana na Singida katika uwanja wa Liti katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliofanyika Novemba 9 ulimalizika kwa sare ya kufungana bao moja.
Wenyeji Singida walipata bao la mapema kupitia kwa Deus Kaseke nasi tulisawazisha kupitia kwa Peter Banda.
Hatujaangusha pointi yoyote….
Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa hatujapoteza wala kupata sare tukiwa tumeshinda mechi zote nne za ligi tulizocheza.