Saa 10 jioni ya leo kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuikabili Pamba Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Tutaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri kutokana nakuwa kileleni mwa msimamo na alama zetu 25.
Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wetu huku tukijua wapo nyumbani lakini tumejipanga na tupo tayari kuhakikisha tunapata ushindi.
Alichosema kocha Fadlu kuelekea mchezo wa leo
Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na wachezaji wapo tayari kuhakikisha pointi tatu zinapatikana.
Kocha Fadlu amesema wachezaji wamefanya mazoezi ya mwisho jana katika Uwanja wa CCM Kirumba na malengo yetu ni kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu ugenini.
“Mechi za ugenini zimekuwa na ugumu kuliko za nyumbani na hii inatokana na uwanja ingawa tumejiandaa kuhakikisha tunapambana ili kupata pointi zote tatu.”
“Ratiba ya mechi za Kalenda ya FIFA haijaharibu maandalizi kuelekea mchezo wetu, wachezaji wengi wametumika kwenye timu zao za Taifa hivyo wapo timamu kimwili na wapo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Pamba,” amesema Kocha Fadlu.
Wachezaji wapo tayari kwa Pamba Jiji…
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amesema wao kama wachezaji wapo tayari kuhakikisha wanapambana hadi mwisho na kufuata maelekezo ya mwalimu ili kuwapa furaha Wanasimba.
“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho, tunafahamu Wanasimba wanahitaji furaha nasi tupo hapa kuhakikisha tunakamilisha furaha yao,” amesema Kapombe.
Ni mara ya kwanza tunakutana na Pamba
Baada ya kupita takribani miaka 24 leo tunakutana na Pamba Jiji katika mechi za ligi Kuu kwakuwa tangu iliposhuka daraja kipindi hicho hatukuwahi kucheza dhidi yao.