Leo tuko Ushirika Moshi kuikabili Polisi Tanzania

Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa Ushirika kuikabili Polisi Tanzania katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tunaingia katika mchezo wa leo tukiwa tunajua tunakutana na timu imara yenye wachezaji bora lakini tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapata ushindi.

Wachezaji wamefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Ushirika jana na wapo kwenye hali nzuri tayari kupambana kupata alama tatu muhimu kwenye mchezo wa leo.

MGUNDA AFUNGUKA KUHUSU HALI YA KIKOSI

Kocha Mkuu Juma Mgunda, amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mchezo wa leo na maandalizi yamekamilika.

Mgunda amesema tunaiheshimu Polisi na tunategemea kupata ushindani mkubwa ingawa hawapo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindani.

“Maandalizi ya mchezo yamekamilika na wachezaji wapo kwenye hali nzuri, tunajua mechi itakuwa ngumu. Ingawa Polisi haipo kwenye nafasi nzuri lakini tutaiheshimu lengo letu ni kupata pointi tatu,” amesema Mgunda.

KANOUTE, MWANUKE WAREJEA

Kiungo mkabaji Sadio Kanoute ambaye aliukosa mchezo uliopita kutokana na kupata maumivu yupo fiti na atakuwa sehemu ya mchezo wa leo.

Winga Jimmyson Mwanuke ambaye alikuwa majeruhi wa muda mrefu nae amerejea kikosini na jana amefanya mazoezi ya mwisho na wenzake ambapo Kocha Juma Mgunda akiona inafaa atamtumia kwenye mchezo wa leo.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER