Kaimu Kocha Mkuu, Daniel Cadena amesema maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Namungo utakaopigwa kesho saa 10 jioni Uwanja wa Uhuru yanaendelea vizuri.
Cadena amesema wachezaji wameandaliwa vizuri kimwili na kiakili kuhakikisha tunacheza vizuri na kupata ushindi.
Cadena ameongeza kuwa ameifuatilia Namungo jinsi inavyocheza na amekiri haitakuwa mechi rahisi lakini tumejipanga kupata matokeo chanya nyumbani.
“Tumewaandaa vizuri wachezaji kwa ajili ya mchezo wa kesho dhidi ya Namungo, tunawaheshimu wapinzani, na tumewafutailia. Tunategemea mchezo mgumu lakini tupo tumejipanga kupata ushindi,” amesema Cadena.
Kwa upande wake nahodha John Bocco amesema kilichopo sasa ni kujipanga kwa mechi zilizo mbele yetu kilichotokea nyuma tumekiacha na kukisahau.
Bocco amewaomba mashabiki kuendelea kuipa sapoti timu bila kuangalia matokeo ya nyuma na wao kama wachezaji watahakikisha wanapambana kuwapa furaha.
“Hatuangalii yaliyopita, tunajipanga kwa kilicho mbele yetu. Ligi bado mbichi kikubwa tunaomba sapoti kutoka kwa mashabiki wetu tunaamini tutarudi kwenye ubora wetu,” John Bocco, Nahodha wa timu.