Kauli ya Kocha Matola kuelekea mchezo dhidi ya Dodoma

Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Dodoma Jiji utakuwa mgumu lakini tumejiandaa kuhakikisha tunafanya vizuri na kuchukua pointi tatu muhimu nyumbani.

Matola amesema haiwezi kuwa mechi rahisi kwakuwa hata Dodoma wanahitaji alama tatu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo lakini tumewaandaa wachezaji vizuri kuhakikisha tunapata matokeo chanya.

Akizungumzia hali ya kikosi Matola amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri huku akiweka wazi kuwa mlinzi wa kati, Che Fondoh Malone ataendelea kukosekana kutokana nakuwa majeruhi lakini mlinda mlango, Moussa Camara amerejea kikosini.

“Haiwezi kuwa mechi rahisi Dodoma wana timu nzuri na mwalimu anayependa ushindani, kikosi chetu kipo tayari kwa kupambana hadi mwisho kutafuta alama tatu muhimu.

“Malengo yetu yanabaki kuwa yale yale ya kushinda kila mchezo, tunajua itakuwa mechi ngumu hasa kwakuwa tunaelekea mwishoni mwa msimu lakini tupo tayari,” amesema Matola.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia David Kameta ‘Duchu’ amesema kwa upande wao wapo tayari kupambana hadi mwisho kuhakikisha ushindi unapatikana na kuwapa furaha Wanasimba.

“Tunaijua vizuri Dodoma Jiji ni timu imara lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo chanya, kwetu kila mchezo ni fainali na malengo yetu ni ubingwa,” amesema Duchu.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER