Kocha Mkuu Didier Gomes, amesema mchezo wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana hautakuwa rahisi hivyo tunapaswa kuchukua tahadhari zote.
Gomes amesema mechi za Ligi ya Mabingwa mara zote zinakuwa ngumu hivyo kwa kuwa tunataka kufika hatua ya makundi tunapaswa kuongeza umakini ili kufanikisha hilo.
Kama ilivyokuwa msimu uliopita, Gomes amesema malengo yetu ni kuendelea kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika kwa hiyo kila mchezo tunauchukulia kwa umuhimu mkubwa.
Mchezo huo utapigwa Oktoba 17 nchini Botswana na marudiano yatakuwa Oktoba 24 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Inapokuwa ni Ligi ya Mabingwa mchezo wowote si rahisi nasi tumelijua hilo, tuna siku sita za kufanya mazoezi kabla ya mechi tutahakikisha tunawapa furaha mashabiki wetu.
“Malengo yetu ni kuendelea kufanya vizuri kwenye michuano hii kwahiyo tutahakikisha kila mchezo tunaupa umuhimu sawa. Mchezo dhidi ya Galaxy utakuwa mgumu lakini tupo tayari kuwakabili,” amesema Gomes.