Kauli ya Kocha Fadlu kuelekea mchezo dhidi ya Stellenbosch

Kocha Mkuu, Fadlu Davids ameweka wazi kuwa mchezo wa kesho wa marudiano wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch utakuwa mgumu zaidi ya ule kwanza tulioishinda bao moja Visiwani Zanzibar.

Fadlu amesema Stellenbosch ni timu ambayo haichezi kwa kumiliki mpira lakini inafanya mashambulizi ya kushtukiza pamoja na kurusha mipira kuelekea golini jambo ambalo tunapaswa kuchukua tahadhari.

Akizungumzia hali ya kikosi, Fadlu amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri na tutaingia katika mchezo wa kesho kwa malengo ya kutafuta bao la ugenini huku tukiwa makini kwenye kuzuia tusiruhusu bao.

“Itakuwa mechi ngumu lakini, malengo yetu ni kuhakikisha tunavuka na kutinga fainali. Tunahitaji sare ya aina yoyote kama ikishindikana kabisa hata bila kufungana lakini tumejipanga kutafuta bao la ugenini ili kuwapa wakati mgumu wapinzani,” amesema Fadlu.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mshambuliaji, Steven Mukwala amesema katika mchezo wa mkondo wa kwanza tuliibuka na ushindi wa bao moja lakini tunahitaji kushinda zaidi ili kutinga fainali.

“Bado kuna dakika 90 za kupambana ili kufikia malengo yetu tuliyojiwekea. Bao moja tuliloshinda nyumbani hatuwezi kusema limetuvusha moja kwa moja tupo tayari kupambana hadi mwisho kuona tunaweza kufika fainali,” amesema Mukwala.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER