Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Azam FC utakuwa mgumu kutokana na ubora walionao wapinzani na aina ya wachezaji waliopo kikosini kwa sasa.
Fadlu amesema ameitazama Azam katika mechi tatu zilizopita chini ya kocha wao mpya na kubaini kuwa wamebadilika kiuchezaji lakini tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri na kuibuka na pointi zote tatu.
Akizungumzia hali ya kikosi kocha Fadlu amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri na tayari kwa mchezo huo inagawa ameweka wazi kuwa tutawakosa viungo wakabaji Yusuph Kagoma na Mzamiru Yassin ambao ni majeruhi.
“Wachezaji wangu wameonyesha jambo chanya katika mchezo uliopita ambapo tulitoka nyuma kwa bao moja na kusawazisha na kuongeza mawili hilo linaongeza morali kwa timu kuelekea mchezo wa kesho,” amesema Kocha Fadlu.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kiungo mshambuliaji Awesu Awesu amesema kila mmoja atakayepata nafasi yupo tayari kuipambania timu na lengo likiwa kuchukua pointi zote tatu.
Awesu ameongeza kuwa amefurahi mechi hiyo kupelekwa katika Zanzibar kwakuwa atakuwa anacheza katika ardhi ya nyumbani na endapo mwalimu atampa nafasi ya kucheza amejipanga kuonyesha uwezo mkubwa.
“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kwa ajili ya mchezo huo, tunaamini utakuwa mgumu lakini tumejipanga na matumaini yetu mashabiki watakuja kwa wingi kutupa sapoti,” amesema Awesu.