Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema maandalizi ya mchezo wa kesho wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini utakaopigwa Uwanja wa Amaan Zanzibar saa 10 jioni yamekamilika.
Fadlu amesema kikosi kipo kwenye hali nzuri na tayari kimezoea mazingira ya Zanzibar na malengo yetu ni kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi nyumbani ili katika mechi ya mzunguko wa pili Afrika Kusini isiwe na presha kwetu.
Fadlu ameongeza kuwa utakuwa mchezo mgumu kwakuwa hata Stellenbosch wanahitaji nafasi ya kufuzu na kutinga fainali lakini tupo tayari kwa vita ya dakika 90 na kufanikisha malengo yetu.
“Kikosi kipo kwenye hali nzuri, tunafahamu haitakuwa mechi rahisi lakini tupo nyumbani na tuna faida yakuwa na mashabiki ambao sina shaka watakuja kwa wingi.
“Kikosi chetu kimezidi kuimarika siku hadi siku, makosa tulivyokuwa tunafanya kuanzia hatua ya awali, makundi mpaka robo fainali yamepungua kwa kiasi kikubwa na tupo tayari kwa ajili ya malengo yetu kama timu ya kuvuka hatua hii,” amesema Fadlu.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kati, Che Fondoh Malone amesema watacheza soka la kawaida bila presha huku lengo likiwa kupata idadi kubwa ya mabao.
Che Malone amesema wanafahamu hatua tulioyopo inaamuliwa na mtaji wa mabao kitu ambacho wamepanga kukifanya kwa asilimia 100 huku pia wakihakikisha haturusu nyavu zetu kuguswa.
“Tutaingia kwa kucheza mpira tuliouzoea, hatutakuwa na presha lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi wa mabao mengi katika uwanja wa nyumbani na hilo litawezekana kama mashabiki watakuja kwa wingi kuja kutushanhilia,” amesema Che Malone.