Tumekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji, Neo Maema kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mkataba wa mwaka mmoja huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwingine mmoja.
Maema (29) raia wa Afrika Kusini ni mchezaji mzoefu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na tunategemea atakuwa msaada mkubwa katika mashindano ya ndani na nje.
Kabla ya kujiunga na Mamelodi, Maema alikuwa akicheza katika klabu ya Bloemfontein Celtic inapatikana katika mji aliozaliwa nchini Afrika Kusini kuanzia mwaka 2018-2021.
Maema amechelewa kujiunga na wenzake kutokana nakuwa wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ iliyokuwa ikishiriki michuano ya CHAN wakiwa kundi C ambalo lilikuwa likicheza mechi zake nchini Uganda huku yeye akiwa ndiye nahodha wa timu.
Maema amecheza mechi zote nne za hatua ya makundi akiwa na Bafana Bafana kwenye michuano ya CHAN huku akifunga bao moja na kusaidia kupatikana kwa jingine moja.
Tayari Maema amejiunga na wachezaji wenzake kambini Cairo nchini Misri kuendelea na maandalizi ya msimu mpya wa mashindano 2025/2026 (Pre Season).