Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa Taifa wa Bingu wa Mutharika hapa Malawi kuikabili Nyasa Big Bullets katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tunaingia katika mchezo wa leo tukifahamu tupo ugenini na tutapata upinzani mkubwa kutoka Bullets lakini tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri.
Tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mchezo wa leo ili kujitengenezea mazingira kwenye mechi ya marudiano itakayofanyika jijini Dar es Salaam wiki ijayo.
KOCHA MGUNDA ATOA NENO
Kocha mkuu wa muda, Juma Mgunda amesema kwa muda mfupi aliokaa na kikosi ameona wachezaji wakielewa mafunzo yake haraka na anaamini Mungu akijalia tutapata matokeo mazuri.
Mgunda amesema wachezaji wote 25 waliopo kikosini wako kwenye hali nzuri na atakuwa na wigo mpana wa kupanga kikosi kwenye mchezo huo ambao tunahitaji kufanya vizuri.
“Nashukuru Mungu wachezaji wapo kwenye hali nzuri wote waliosafiri wamefanya mazoezi ya mwisho jana tayari kwa mechi.
“Tunajua tupo ugenini tumewaandaa wachezaji kisaiokojia kwa kitakachotokea ndani na nje ya uwanja kwa kuwa lengo letu ni kupata matokeo mazuri,” amesema Mgunda.
ZIMBWE JR AFUNGUKA
Kwa uoande wake Nahodha Msaidizi Mohamed Hussein, amesema wachezaji wapo tayari kimwili na kiakili kuhakikisha tunapigania nembo ya timu ili kuwapa furaha Wanasimba na Watanzania kwa ujumla.
“Sisi wachezaji tupo tayari kuhakikisha tunapambana mpaka jasho la mwisho kufanya vizuri kwa ajili ya timu na furaha kwa Wanasimba,” amesema Zimbwe Jr.