Jayrutty yaingia ushirikiano na Diadora kutengeneza vifaa vya Michezo vya klabu

Kampuni ya Jayrutty imeingia ushirikiano na Kampuni ya kutengeneza vifaa vya michezo ya nchini Italia ya Diadora kwa ajili ya kuzalisha na kusambaza vifaa vya michezo vyaklabu yetu katika kipindi chote cha miaka mitano ya mkataba wetu.

Ushirikiano huu unaifanya Simba kuwa miongoni mwa timu inayovaa jezi zinazotengenezwa na Kampuni hiyo ya Kimataifa ya Diadora kama ilivyokuwa kwa Klabu ya AS Roma na timu ya Taifa ya Italia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jayrutty, Joseph Rwegasira amesema lengo la makubaliano hayo ni kuhakikisha Simba inavaa jezi bora za kimataifa ambazo zitaendana na ukubwa wa chapa yetu kwa sasa.

Nae Mkurugenzi wa Diadora Ukanda wa Kusini mwa Afrika SADC, Bw. Yusuph Wadi amesema wamekuwa na uzoefu mkubwa na kuzalisha vifaa vya michezo vyenye ubora kwa miaka mingi na wapo tayari kuhakikisha wanaipandisha chapa ya Simba Kimataifa.

“Diadora imefanya kazi na timu kubwa duniani kama As Roma, Timu ya Taifa ya Italia na nyinginezo na tunaamini ushirikiano huu utakuwa na faida kwa pande zote na tupo hapa kuona tunapandisha thamani ya chapa ya Simba,” amesema Bw. Wadi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Klabu, Bi. Zubeda Sakuru amesema malengo ya ushirikiano huu ni kuhakikisha klabu yetu inafikia malengo iliyojiwekea.

Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu ameishukuru Jayrutty kwa kuingia makubaliano hayo na Kampuni ya Diadora huku akiwaomba Wanasimba wote kuwapa ushirikiano na kununua bidhaa halisi zenye chapa hiyo.

“Kwa upande wa klabu ya Simba kwanza tumefurahi kwa ushirikiano huu mkubwa, tunaenda kuweka historia ya kuvalishwa na moja ya chapa kubwa duniani ya Diadora kikubwa nawaomba Wanasimba tuwape ushirikiano,” amesema Mangungu.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Naibu Waziri Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Mh. Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ amesema amefurahishwa na jinsi Kampuni ya Jayrutty inavyotimiza kwa vitendo makubaliano ya mkataba iliyoingia na klabu na kuonyesha mwanga bora wa mafanikio.

“Wiki mbili zilizopita nilikuwepo wakati wa kutiliana saini ya mikataba na leo nipo kushuhudia yale makubaliano yakitimizwa kwa vitendo hili limenifurahisha binafsi na kwa niaba ya Serikali tunaamini hii itakuwa ni dira ya maendeleo ya soka nchini,” amesema Mh. Mwana FA.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER