Na Ezekiel Kamwaga
NIMEMALIZA kuzungumza kwa simu na mwandishi kutoka Malawi, Brighton Kanyama, na ameniuliza jambo moja tu; Simba Day ni lini? Kwa maelezo yake mwenyewe, anatamani kuja kushuhudia.
Kwa miaka mitatu au minne iliyopita, amekuwa akiona tu kwenye mitandao ya kijamii lakini mwaka huu – mara baada ya kusikia Duncan Nyoni na Peter Banda wamekuja Tanzania; wahka umempaa.
Anataka kuja Dar es Salaam kuwaona Wekundu wa Msimbazi. Anataka kupata raha.
Na anasema hayuko peke yake. Wako Wamalawi wengine ambao wangetamani kuja kuiona Simba katika Simba Day.
Jana mchana, nimepokea email kutoka gazeti moja la Senegal likiuliza kama Simba ni timu inayomilikiwa na Jeshi au mtu mmoja. Nimempa maelezo ya kutosha. Kwa mara ya kwanza katika historia ya soka, Wasenegali wameanza kuzungumza kuhusu Simba.
Kuna mchapo mmoja mashuhuri nchini Zambia kuhusu ujio wa Rally Bwalya kuja Simba. Inasemwa kuna timu ilimtaka kabisa. Wakakubaliana kila kitu. Lakini alipojua Simba inamtaka, akawaambia viongozi wa timu yake kwamba anataka kuja kucheza Msimbazi.
Na viongozi wake wakamwambia amefanya uamuzi sahihi. Kwao, katika eneo hili la Afrika Mashariki na Kati, kuna timu moja inayokusanya vipaji na kuonesha dalili ya kwenda mbele – Lunyasi.
Mitandaoni, huko Ulaya na Marekani, kuna watu wanajiuliza inakuwaje klabu ya Afrika inaongeza washabiki mitandaoni kwa spidi ya sasa. Kwa sasa, katika Instagram pekee Simba inakaribia kufuatiliwa na watu zaidi ya milioni tatu. Na hili jambo limeanza kuwa namna hii katika miaka mitatu tu iliyopita.
Wana Simba wenyewe wako na furaha. Wanasapoti timu yao kwa kila hali na mali. Kuna akina Mo Dewji na Profesa Janabi. Kuna akina Musleh Ruweihy na Mwina Kaduguda. Wakati huohuo, kuna akina Kay Mziwanda na akina Justine Mwakitalima.
Wote hao ni Simba.
Kila nikitazama Simba ilipo sasa, naona kule tunakokwenda ni kukubwa zaidi. Unafahamu kwanini Manchester United na Real Madrid ni kubwa sana hivi sasa? Ni kwa sababu zilitoka kuwa timu za mataifa yao kuja kuwa timu za dunia.
Manchester United walianza kuvuna jirani kwa kuwaleta akina George Best; unaanzia ukubwa wa nyumbani kwanza. Halafu kwenye ukuu wake kwenye miaka ya 1990, ikaanza kuvuna kwa kuwachukua akina Eric Cantona na wengine kutoka nje ya Uingereza. Baadaye, ikawa ikawavutia akina Cristiano Ronaldo, Dwight Yorke, Park Ji Sung, Quinton Fortune na wengine kutoka dunia nzima.
Madrid ndiyo usiseme. Na Barcelona. Na Bayern Munich. Na wengine wengi wakubwa.
Matokeo yake, sasa Manchester United inaweza kwenda Japan na kujaza uwanja. Inaweza kwenda Marekani na kujaza uwanja.
Namtazama Aishi Manula. Namwangalia Mohamed Hussein. Nawatazama nyota kama Banda, Pape Ousmane Sakho, Bwalya, Nyoni na wengine na kuona namna nyavu za Simba zilivyoanza kutwekwa mbali kabisa.
Ipo siku Simba itapiga mpira ambao utaanza kuzungumzwa Afrika nzima. Iko siku, Simba itakuja kuwa kama Real Madrid au Manchester United ya Afrika.
Wazambia watatamani kumwona Rally. Wamalawi akina Nyoni. Waganda watasema Taddeo Lwanga na Wakenya watasema nani hataki kumwona Ochieng akiwa anafanya yake.
Naiona barua ikiomba Simba Day ifanyikie nje ya Tanzania. Nani ambaye ataacha kwenda kuona klabu au timu ambayo inatoa burudani ndani na nje ya uwanja ikizindua msimu mpya kwao?
Kwa mitandao hii ya sasa, kwa wachezaji hawa ambao sasa hawataki kwenda kwingine zaidi ya Simba na kwa mafanikio ambayo yameanza kuonekana, jambo hili wala haliko mbali.
Wengine Afrika ambao wanatamba sasa au waliwahi kutamba huko nyuma, hawakuwa na mbinu na mikakati mikubwa ya kujitanua Afrika nzima kama ambavyo Simba inayo sasa.
Wao waliona inatosha kuwa wakubwa kwao. Na hawana kitu walau kinachokaribiana na Simba Day. Huu ni upepo wa kisulisuli.
Kaeni tu mkao wa kula. Kuna siku mtapanda ndege na mabasi kwenda kuona Simba Day nyingine.
Ipo siku!!!!!
Mwisho
2 Responses
Huyu ndio kamwaga ninaemjua,andiko zuri Sana na lenye kuonesha wapi Simba ilipo na wapi inapoelekea,Mwenyezi Mungu atuongoze tufikie malengo Yetu inshallah
Yeah yeah