Ushindi wa bao moja tuliopata jana dhidi ya Singida Black Stars ugenini ulikuwa mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/25.
Hii ina maana kuwa tumecheza na timu zote 15 zilizopo kwenye ligi msimu huu huku tukiwa na asilimia 87 ya ushindi kwenye mechi hizo.
Pamoja na kuwa na kikosi ambacho asilimia kubwa ya wachezaji wake ni wageni lakini wameweza kupigania timu kupata ushindi katika mechi nyingi kuliko timu yoyote katika mzunguko wa kwanza wa Ligi.
Tumemaliza Mzunguko tukiwa kileleni…..
Ushindi wa jana dhidi ya Singida Black Stars umetufanya kufikisha alama 40 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote katika mzunguko huu wa kwanza.
Katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza tumeshinda michezo 13 tukitoka sare moja na kupoteza moja.
Tumemaliza tukiwa vinara wa ufungaji…
Bao pekee lililofungwa jana na kiungo mkabaji Fabrice Ngoma katika ushindi dhidi ya Singida Black Stars likikuwa la 31 kufungwa kwenye mzunguko wa kwanza.
Tumefanikiwa kufunga mabao hayo huku tukiruhusu mabao matano yakiwa ndio machache zaidi kufungwa kwenye mzunguko wa kwanza.
Jean Charles Ahoua ndiye kinara kikosini…
Kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua ndiye kinara wa ufungaji kwenye kikosi chetu akitupia mabao saba akizidiwa moja na anayeongoza Elvis Rupia.
Pamoja na kufunga mabao hayo pia amesaidia kupatikana kwa mengine matano (Assisti).
Camara acheza mechi zote….
Mlinda mlango Moussa Camara ndiye mchezaji pekee kwenye kikosi chetu kucheza mechi zote 15 za mzunguko wa kwanza wa Ligi bila kufanyiwa mabadiliko.
Hii ina maana Camara raia wa Guinea amecheza dakika 1350 akiwa ameruhusu kufungwa katika mechi tatu pekee akiwa na Cleansheet 12.