Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomez da Rosa, amesema kambi ya Morocco ni msingi muhimu wa maandalizi ya msimu ujao wa mashindano unaoanza mwezi huu.
Akizungumza na Simba App, Gomez alisema baada ya Morocco sasa anajua nini cha kufanya kuanzia sasa kuelekea mwanzoni mwa msimu.
“Kwa mwalimu, mazoezi ya pre season ni muhimu kwa sababu yanakupa nafasi ya kukaa na wachezaji kwa muda mrefu na kuwafahamu.
” Kimazoezi, wachezaji pia wanapata nafasi ya kujenga utimamu wa kimwili ambao utawasaidia wakati mashindano yatapoanza. Kama wachezaji hawako fiti kabla msimu haujaanza, ni vigumu kuanza msimu vizuri,” alisema.
Gomez alitumia pia nafasi hiyo kueleza kwamba mazoezi ya Morocco yamempa tu mwanzo mzuri lakini bado programu yake haijamalizika.
Simba imerejea Tanzania baada ya kumaliza kwa awamu ya kwanza ya pre season ambayo kwa kiasi kikubwa iliathiriwa na kitendo cha nyota wake 13 kuitwa katika timu mbalimbali za taifa barani Afrika.
Kwa mujibu wa Gomez, kikosi kilichobaki kitaendelea na mazoezi wiki hii katika siku na sehemu itakapotangazwa na klabu.
Kocha huyo ambaye tayari ameipa Simba mataji mawili tangu achukue nafasi hiyo msimu uliopita, amesema anatarajia kutumia baadhi ya wachezaji kutoka timu ya vijana ya Simba kwenye mazoezi yatakayoanza ili kuziba upungufu wa wachezaji wenye majukumu kwenye timu za taifa na wenye dharura nyingine.