Kocha Mkuu Didier Gomez leo ataongoza mazoezi baada ya kurejea kutoka mapumziko ya siku chache kutokana na kusimama kwa ligi kupisha mechi za kirafiki za kimataifa za timu za taifa.
Kwa muda wote Gomez alipokuwa mapumziko huku Kocha Msaidizi Seleman Matola naye alikuwa katika majukumu ya Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) hivyo Kocha wa Viungo Adel Zrane alishika usukani wa kuongoza mazoezi.
Wachezaji ambao walikuwa hawajaitwa kwenye timu zao za taifa ndiyo wataendelea na mazoezi katika viwanja vyetu vya Mo Simba Arena vilivyopo Bunju.
Nyota wetu ambao walikuwa kwenye kikosi cha Taifa Stars pamoja na Kocha Matola wao wataanza mazoezi kesho huku wale waliokuwa wameenda kuziwakilisha nchi zao kama Taddeo Lwanga, Medie Kagere na Rally Bwalya wakitarajiwa kutua nchini muda wowote kuanzia sasa.
Timu yetu inajiandaa na michezo ya ligi kuu dhidi ya Polisi Tanzania Juni 19 kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza kisha Mbeya City katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Juni 22, mwaka huu.
Baada ya mechi hizo kikosi kitapaa kuelekea Songea kuikabili Azam FC katika mechi ya Nusu Fainali ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) utakaopigwa Uwanja wa Majimaji kati ya Juni 26 mwaka huu.