Kocha Mkuu Didier Gomes, amesema mchezo wa kesho wa kirafiki dhidi ya TP Mazembe kwenye kilele cha Simba Day utakuwa mgumu lakini utakuwa kipimo kizuri kwetu.
Gomes amesema mchezo wa kesho utatupa picha kuelekea msimu mpya wa ligi 2021/22 pia kuelekea mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga wiki ijayo.
Amesema atafurahi kucheza mbele ya mashabiki wengi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo tutahakikisha tunafanya kila linalowezekana kupata ushindi.
“Mazembe ni timu bora na ina historia kubwa barani Afrika, kwanza nawashukuru kwa kukubali kuja kucheza nasi kwenye Simba Day. Ni mechi itakayokuwa kipimo kizuri kwetu kuelekea msimu mpya wa ligi.
“Tuna furaha kukutana na mashabiki wetu kesho, tuna imani uwanja utajaa nasi tumejiandaa kuhakikisha tunawapa burudani na zaidi kushinda,” amesema Kocha Gomes.
Kwa upande wake Nahodha John Bocco amesema wachezaji wamepata maandalizi ya kutosha na kesho wamejipanga kuonyesha uwezo wao ili kuwafurahisha mashabiki.
“Tumepata maandalizi mazuri, TP Mazembe ni timu kubwa Afrika runaamini itakuwa kipimo kizuri kuelekea msimu mpya wa ligi. Sisi wachezaji tumejipanga kuhakikisha tunaonyesha uwezo wetu kuwafurahisha mashabiki kikubwa wajitokeze kwa wingi,” amesema Bocco.
One Response