Kocha Mkuu, Didier Gomes ameweka wazi kuwa kwenye soka kila kitu kinawezekana hivyo tunapaswa kupambana kuhakikisha tunapindua matokeo na kutinga Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha Gomes ameyasema hayo baada ya mazoezi ya leo jioni katika Viwanja vya Mo Simba Arena ambapo amekiri kuwa haitakuwa kazi rahisi lakini inawezekana na hatimaye tufuzu nusu fainali.
Jumamosi ya Mei 22 kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Kaizer Chiefs kwenye mchezo ambao tunatakiwa kushinda mabao 5-0 ili kutinga Nusu Fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Gomes amesema katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Johannesburg wiki iliyopita hatukucheza vizuri hasa kwenye safu ya ulinzi kitu ambacho benchi la ufundi linakifanyia kazi kuondoa makosa yote.
“Tunapaswa kupambana kiume, wachezaji, benchi la ufundi, viongozi pamoja na mashabiki tunatakiwa kujua kwenye mpira kila kitu kinawezekana na tunajiandaa kufanya hivyo.
“Nakubali hatukucheza vizuri kwenye mchezo wa kwanza hasa katika safu ya ulinzi lakini tunaendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza mazoezini ili tusiyarudie tena,” amesema Gomes.
One Response
Mko vizuri