Fadlu: Tumepata muda mzuri kujiandaa dhidi ya Namungo

Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema baada ya mchezo wetu dhidi ya Dodoma Jiji kuahirishwa wikiendi iliyopita kikosi chetu kimepata muda mrefu wa kujiandaa kabla ya kesho kukutana na Namungo FC katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Fadlu amesema kabla ya kikosi kufika Ruangwa jana kilipata muda wa kufanya mazoezi na leo pia kitafanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Majaliwa kabla ya kuivaa Namungo kesho.

Akizungumzia mchezo wenyewe, Fadlu amesema utakuwa mgumu hasa baada ya wapinzani kuzidi kuimarika huku akiweka wazi uwepo wa kocha mzoefu, Juma Mgunda utazidi kuifanya mechi kuwa ya ushindani.

Fadlu ameongeza kuwa lengo la kwanza kwenye mchezo wa kesho ni kupata alama tatu na la pili ni kuhakikisha tunapata mabao mengi ambayo yatatawanyika kila eneo bila kutegemea mchezaji mmoja.

“Mpango wetu ni kuhakikisha magoli yanapatikana pande zote ndio maana unaona walinzi Shomari Kapombe na Mohamed Hussein wanahusika kwenye kufunga na kutoa ‘asisti’ viungo na washambuliaji ni jukumu lao pia lakini hatutaki kuwapa presha wachezaji wetu,” amesema Fadlu.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia, David Kameta ‘Duchu’ amesema tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Namungo lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda na kupata alama tatu ugenini.

Duchu ameongeza kuwa tumekuwa tukipata wakati mgumu tunapokutana na Namungo katika uwanja wa Majaliwa lakini tupo tayari kupambana hadi mwisho ili kufanikisha malengo.

“Mchezo dhidi ya Namungo haujawahi kuwa rahisi, katika miaka miwili iliyopita hatujapata ushindi hapa lakini tumekuja kamili kuhakikisha tunashinda,” amesema Duchu.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER