Kocha Mkuu, Fadlu Davids ameweka wazi kuwa kuelekea mchezo wa kesho wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani wa jadi Yanga hatuna presha na tupo tayari kuhakikisha tunashinda.
Fadlu amesema tumekuwa na wakati mzuri katika maandalizi yetu ya kuanza msimu (Pre Season) na tumesajili wachezaji bora ambao tunaamini watatupa matokeo chanya.
Fadlu ameongeza utakuwa mchezo mgumu hasa ukizingatia tunakutana na timu imara huku ikiwa ni mechi ya Derbi lakini tumejipanga na tupo tayari kuhakikisha tunawapa furaha mashabiki wetu.
“Kwa upande wetu hatuna presha kuelekea mchezo wa kesho, tunafahamu utakuwa mgumu kutokana na aina ya wapinzani tunaoenda kukutana nao kwahiyo kwa ujumla tupo tayari kwa Ngao ya Jamii,” amesema Fadlu.
Kwa upande wake nahodha wa timu, Shomari Kapombe amesema wao kama wachezaji wapo tayari kuhakikisha wanafuata maelekezo ya walimu watakayopewa ili kupata ushindi.
Kapombe ameupongeza Uongozi wa klabu na benchi la ufundi kwa kufanya usajili mzuri ambao anaamini utarejesha nyakati za furaha ambazo tumezipoteza kwa muda mrefu.
“Kwetu sisi wachezaji naweza kusema tupo tayari, kila atakayepata nafasi atakuwa tayari kutoa asilimia 100 ili kuiwezesha timu kupata ushindi,” amesema Kapombe.