Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Bonanza, Mbunge wa Makete, Festo Sanga amesema Bonanza la mwaka huu litafanyika Februari Mosi na kama kawaida litashirikisha mashabiki wa timu za Simba na Yanga kutoka katika Taasisi mbalimbali jijini Dodoma.
Sanga amesema lengo la Bonanza hilo ni kuhakikisha afya zinaimarika kwakuwa kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Afya magonjwa yasioambuzika ndio yanayoongoza kwa kuwasumbua watu.
“Mwaka huu tumekuja kivingine michezo itakuwa mingi ili kuimarisha afya zetu na hicho ndicho kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita,” amesema Sanga.
Nae Mgeni Rasmi wa Bonanza hilo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema timu za Simba na Yanga zimekuwa zikimpa heshima kubwa nje ya nchi na anaamini siku moja miamba hiyo itacheza mechi ya Super Cup.
“Simba na Yanga ni timu zenye heshima kubwa chochote inachofanya lazima kiwe kikubwa hata baada ya kupokea mualiko huu nimeona nije mwenyewe bila kutuma mwakilishi ili kuonyesha thamani ya jambo lenyewe,” amesema Rais Karia.
Kwa upande wake Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amesema katika kila shindano ambalo tunaloshiriki lengo ni moja kutwaa ubingwa.
Ahmed amesema msimu uliopita kwenye Bunge Bonanza tulikuwa Mabingwa wa jumla lakini tulipoteza kwenye mpira wa miguu lakini sasa hatutataka kurudia kilichotokea.
“Sisi ndio Mabingwa wa jumla, unajua kushinda michuano ya Mpira wa mikono, Mpira wa wavu, kuvuta kamba na kuogelea ni jambo zuri sana lakini mpira wa miguu ndio kilele kwahiyo msimu huu tunakata kushinda michezo yote,” amesema Ahmed.