Mlinda mlango namba tatu, Ally Salim amesema baada ya kupangwa kwenye mchezo wa Derby dhidi ya Yanga alitumiwa ujumbe na Aishi Manula kumtakia kheri.
Ally amesema mbali na kumtakia kheri ya mchezo mzuri Manula pia alimtaka aiswe na wasiwasi na afanye kama anavyofanyaga mazoezini.
Akizungumzia mchezo ulivyokuwa, Ally amesema hakuwa na wasiwasi wala presha alikuwa anaamini siku moja itatokea na kupata nafasi ya kucheza hivyo alijiandaa.
“Kwanza baada ya kuambiwa nitaanza kwenye mchezo huu mkubwa, kaka angu Aishi alinitumia ujumbe kuniambia nisiwe na wasiwasi nijiamini na alikuwa anaamini nitafanya vizuri.
“Sisi ni binadamu nilikuwa najua kuna siku kaka zangu Aishi na Beno Kakolanya watapata changamoto nami nitapata nafasi ya kucheza hivyo kila siku nilikuwa najiandaa mazoezini,” amesema Ally.