Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema pamoja na ubora walionao Coastal Union lakini tumejipanga kuhakikisha tunapambana ili kupata alama tatu kwenye mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC utakaopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Matola amesema mchezo dhidi ya Coastal haujawahi kuwa mwepesi lakini tupo tayari kupambana mpaka mwisho ili kuweza kuwafurahisha mashabiki wetu.
Matola ameweka wazi kuwa katika mchezo wa kesho tutakosa huduma ya mlinda mlango Moussa Camara na mlinzi wa kati Che Fondoh Malone ambao walipata majeraha kwenye mechi iliyopita dhidi ya Azam FC.
Akizungumzia hali ya kikosi Matola amesema wachezaji wote 22 tuliosafiri nao kutoka Dar es Salaam wapo tayari kwa ajili ya mchezo na tuna matumaini makubwa ya kupata alama zote tatu.
“Tumejiandaa vizuri na mchezo wa kesho dhidi ya Coastal. Tumewaandaa wachezaji kimwili na kiakili kuelekea mchezo huo ambao tunafahamu utakuwa mgumu.”
“Mchezo dhidi ya Coastal haujawahi kuwa mwepesi lakini tutahakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea,” amesema Matola.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji nahodha wa timu Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema tumekuja Arusha kwa lengo moja la kutafuta alama tatu.
“Tumekuja kwenye mchezo huu wa ugenini kutafuta alama tatu hilo ndio jambo muhimu bila kuangalia matokeo yoyote ya nyuma kwani hayo yameshapita,” amesema Zimbwe Jr.