Kocha Mkuu, Fadlu Davids ameweka wazi kuwa mchezo wa kesho wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane utakuwa mgumu zaidi ya mechi nyingine tulizocheza kwenye mashindano haya msimu huu.
Fadlu amesema tunaenda kukutana na timu yenye uzoefu wa mashindano haya na wapo kwenye kiwango bora kwa sasa lakini tumejipanga kuchukua tahadhari zote zinazotakiwa ili kuwadhibiti.
Fadlu ameongeza kuwa amewaandaa wachezaji kiakili kuwa watakutana na mashambulizi ya haraka haraka kutoka kwa Berkane na wanatakiwa kuwa wastahimilivu na watulivu ili kuweza kupata kupata matokeo chanya.
“Tumejipanga kikamilifu kwa ajili ya mchezo wa fainali kesho, kikosi chetu ni kichanga kwenye michuano hii ukilinganisha na wapinzani wetu lakini tumejipanga vizuri na malengo yetu ni kushinda taji hili,” amesema Fadlu.
Nae mlinzi wa kati, Che Fondoh Malone amesema ubingwa wa michuano hii ni fahari ya kila mchezaji wa Simba na wapo tayari kupambana hadi mwisho kuhakikisha wanakuwa sehemu ya kikosi kilichoweka historia ya kuchukua ubingwa.
“Kila mchezaji ana ndoto ya kucheza fainali ya michuano hii mikubwa Afrika, tunafahamu tunaenda kukutana na mpinzani mkubwa lakini tupo tayari kupambana hadi mwisho kufanikisha malengo ya timu,” amesema Che Malone.