Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema tutaingia na mipango ile ile katika mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Tanzania Prisons lengo likiwa kutafuta alama tatu.
Fadlu amesema licha ya kutoka sare ya kufungana bao moja katika mchezo uliopita dhidi ya Fountain Gate FC mipango yetu itakuwa kuhakikisha tunapata mabao ya mapema.
Fadlu ameongeza kuwa kikosi kimefanya mazoezi kamili jana na leo pia kitafanya kuelekea mchezo huo huku akiweka wazi kuwa wachezaji wapo kwenye hali nzuri.
“Tunategemea utakuwa mchezo mgumu, Prisons wana kocha mpya na pia hawako kwenye nafasi nzuri hivyo tumejiandaa kupata upinzani mkubwa lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Fadlu.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amesema pamoja na sare tuliyopata kwenye mchezo uliopita lakini bado malengo yetu ni kupigania ubingwa.
“Sisi kama wachezaji bado hatujakata tamaa na malengo yetu kama tulivyoanza msimu licha ya sare iliyopita lakini tupo tayari kupambana ili kupata alama tatu muhimu,” amesema Kapombe.