Kocha wa Makipa, Daniel Cadena amesema kikosi chetu kipo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya JKT Tanzania utakaopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo saa 10 jioni.
Cadena amesema licha ya ratiba kuwa ngumu kutokana na kucheza mechi kila baada ya siku mbili tumejipanga vizuri kuhakikisha tunawapa furaha mashabiki kwa kupata pointi tatu.
Cadena ameongeza kuwa utakuwa mchezo mgumu hasa ukizingatia wapinzani wetu hawapo kwenye nafasi nzuri lakini tupo tayari kuwakabili.
“Tunajivunia kuwa na wachezaji bora ambao wanacheza kila baada ya muda lakini wanapambana na kuhakikisha tunapata ushindi.”
“Nategemea kuwaona mashabiki wetu wengi kesho uwanjani na tunajua wanahitaji furaha nasi tutajitahidi kuhakikisha tunawapatia,” amesema Kocha Cadena.
Nae nahodha, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema wachezaji wote wapo timamu kimwili na kiakili kuhakikisha wanapambana ili pointi tatu zipatikane kesho.
“Haitakuwa mechi rahisi, tunawajua JKT ni timu nzuri lakini tumejipanga na tutaingia kwenye mchezo wa kesho kwa lengo la kutafuta pointi tatu,” amesema Zimbwe Jr.