Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amewasisitiza mashabiki na wapenzi wetu kutokata tamaa kufuatia kupoteza mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry.
Ahmed amesema kwa sasa kila Mwanasimba anatakiwa kuwa na ajenda moja tu ya kuhakikisha anakata tiketi yake ili kuhudhuria mchezo wa marudiano utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumatano Aprili 9 saa 10 jioni.
Ahmed amesema katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kila kitu tumefanya na hakuna ambacho kinashindikana hivyo tunatakiwa kushikana ili kuiwezesha timu kuvuka na kutinga nusu fainali.
“Kwa hapa tulipofika hatuhitaji Mwanasimba muoga, katika Uwanja wa Benjamin hatuwezi kushindwa kupata mabao matatu hilo kila mmoja anatakiwa kulijua.
“Tumewahi kuifunga Horoya mabao saba, Jwaneng mabao sita na pia tuliwa kwenda mapumziko tukiwa nyuma mabao matatu lakini kipindi cha pili tulirudisha yote na hiyo ndio Simba inapotaka jambo lake,” amesema Ahmed.
Ahmed ameongeza kwa kusema “lengo letu lakuwa hapa Mbezi ni kuwahamasisha Wanasimba kuhakikisha ikifika Jumatano hakuna atayekaa nyumbani wote twendeni Benjamin Mkapa kwa ajili ya kuisapoti timu yetu na safari hii tunavuka na kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.”