Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amesema malengo yetu msimu huu ni kuhakikisha tunavuka hatua ya robo fainali na kutinga nusu fainali.
Ahmed amesema tumepangwa na mpinzani mgumu ambaye ni Al Masry lakini tumejiandaa kuhakikisha tunavuka kihunzi hicho.
Ahmed ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa mchezo tumekuja na kauli mbiu Maalum inayofahamika kuwa ‘Hii tunavuka’ ambayo itaongeza hamasa kwa wachezaji, mashabiki ili kufanikisha malengo yetu msimu huu.
“Kwa miaka mitano mfululizo tumekuwa tukiishia robo fainali kwenye michuano ya Afrika lakini safari hii tumedhamiria kuhakikisha tunavuka.
“Tumekuja na kauli mbiu ya ‘Hii tunavuka’ kwakuwa malengo yetu ni kuvuka na kwa namna yoyote tumejiandaa kulitimiza hilo msimu huu,” amesema Ahmed.
Ahmed ameongeza kuwa kikosi chetu kitaondoka nchini alfajiri ya Ijumaa, Machi 28 kuelekea Misri tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Aprili 2.