Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amesema mara zote tumekuwa tukithamini na kushirikiana na jamii katika kusaidia jamii yenye uhitaji lengo likiwa ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.
Ahmed ametoa kauli hiyo wakati wa chakula cha mchana na watoto yatima kwenye Kituo cha Umra Orphanage Center kilichopo Magomeni Mikumi ikiwa ni moja ya Shughuli za Kijamii kuelekea kilele cha Simba Day, Jumatano ijayo.
Ahmed ameongeza kuwa Simba imekuwa na utaratibu wa kuwa karibu na makundi maalum kama watoto yatima kwakuwa inaamini huku ndani ya jamii hiyo pia wapo mashabiki wa timu yetu.
“Tumekuja hapa kwa malengo mawili, kwanza ni kujiweka karibu na jamii inayotuzunguka, ambapo tunaamini ndani yake kuna mashabiki wa Simba.
“Lengo la pili ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu kwa kuwalisha yatima, hata kama ni mara moja kwa siku, hakuna jambo dogo mbele za Mwenyezi Mungu, kwani malipo yake ni ulinzi na baraka kwa timu,” amesema Ahmed.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Dkt. Seif Muba amewasisitiza Wanasimba mmoja mmoja au vikundi kuendelea kusaidia jamii zenye uhitaji kwakuwa inazidi kutuweka karibu na baraka za Mwenyezi Mungu.
“Sisi kama Viongozi wa Klabu tumekuja hapa kwa ajili ya kurejesha kwa jamii na Wanasimba wengine kwenye maeneo yenu nanyi mfanye kama hivi ili tuendelee kupata baraka za Mwenyezi Mungu,” amesema Dkt. Muba.