Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amewaomba mashabiki kujitokeza uwanjani kesho katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry utakaopigwa Benjamin Mkapa saa 10 jioni.
Ahmed amesema ameyasema hayo muda mfupi baada ya kuzindua Tawi la Simba Azimio, Tandika ambapo amesema mchezo wa kesho ni muhimu kwa kila Mwanasimba hivyo tunapaswa kuhakikisha tunafanikiwa kutinga nusu fainali.
Ahmed amesema itakuwa jambo la ajabu kwa mashabiki kutoka Tunduma, Mwanza, Mbeya na mikoa mingine kuja uwanjani wakati watu kutoka Temeke wapo majumbani wanatazama kupitia luninga.
“Kila zama ina kitu cha kujivunia, sisi wa zama za sasa tunatakiwa kuipeleka Simba nusu fainali ya Kombe la Shirikisho. Imetosha kujivunia historia ya mwaka 1993 na 2003 sasa ni wakati wa kuipeleka Simba nusu fainali na ‘hii tunavuka’,” amesema Ahmed.
Ahmed ameongeza kuwa”Ni wakati wa sasa wa kuandika historia yetu ili tujivunie. Na wenzetu wazamani kuna kazi kubwa waliifanya ili kufanikiwa, na moja ya kazi hiyo ni kuujaza Uwanja wa Uhuru na mashabiki waliingia saa mbili asubuhi, sisi kesho tunaenda kuandika historia yetu.”