Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu Ahmed Ally amewaomba Wanasimba kutoka Kibamba kujitokeza kwa wingi kwenye Tamasha letu la Simba Day litakalofanyika Septemba 10 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ahmed ameyasema hayo wakati wa kuzindua Tawi la Simba lililopo Kibamba ikiwa ni sehemu ya Maandalizi kuelekea Simba Day.
“Ndugu zangu Wanasimba wa Kibamba tupo kwenye Wiki ya Simba, leo ni siku maalumu ya uzinduzi wa Matawi, tumeanzia hapa alafu tutakwenda Bunju na kumalizia Kunduchi. Nichukue nafasi hii kuwataka Wanasimba nchi nzima kujikusanya na kwenda hospitali ya karibu kujitolea damu.”
“Katika wiki hii ya Simba tunafanya matendo ya kumpendeza Mungu kwa maana ya kuwasaidia watoto yatima, kuwasaidia wazee na wajane. Nawasihi Wanasimba wa Kibamba kwenda kutoa kwa jamii na baraka zake zinakuja moja kwa moja kwenye klabu ya Simba,” amesema Ahmed.
Ahmed ameongeza kuwa Simba Day ya mwaka huu ni ya tofauti na burudani zimeongezwa na kila atakaye hudhuria hata jutia muda wake pamoja na pesa yake ya kiingilio.
“Ndugu zangu mwaka huu tumewaandalizia mambo makubwa yani unaingia unakuta burudani na hadi unatoka unapata burudani. Natoa agizo kwa Matawi yote ya Simba ni marufuku Simba Day kuwasha TV ya tawini, wanachama wote waje uwnajani. Shughuli pekee ya tawini ni kukutana asubuhi ili kwenda uwanjani,” amesema Ahmed.