Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu, Ahmed Ally amesema tutatumia mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku kumuaga kiungo wetu Rally Bwalya ambaye tumemuuza kwa timu moja ambayo itatangazwa baadaye.
Ahmed amesema mchezo wa kesho utakuwa wa mwisho kwa Bwalya ndani ya kikosi chetu kwa kuwa baada ya hapo atarudi nyumbani kwao Zambia kujiandaa kujiunga na timu yake mpya.
Ahmed amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kuja kuonyesha heshima kwa Bwalya kutokana na mchango wake mkubwa aliutoa kwa timu.
“Jana tulitoa taarifa kuwa tumemuuza kiungo wetu, Rally Bwalya kwa hiyo kesho tutamuaga rasmi katika mchezo dhidi ya KMC kwa sababu baada ya hapo hatacheza tena akiwa na kikosi chetu.
“Niendelee kuwasisitiza Wanasimba wenzangu tujitokeze kwa wingi uwanjani kuonyesha heshima kwa kiungo wetu Bwalya,” amesema Ahmed.