Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa CCM Kirumba kuikabili Geita Gold katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Kipaumbele chetu cha kwanza katika kila mechi iliyobaki ni kukusanya alama tatu ingawa tunafahamu ni ngumu sababu kila timu inataka kumaliza vizuri msimu.
Tunaiheshimu Geita kutokana na ubora wake na aina ya kikosi walicho nacho lakini tumejiandaa kuhakikisha tunashinda.
KAULI YA PABLO KUHUSU MCHEZO WA LEO
Kocha Mkuu Pablo Franco ameweka wazi kuwa mchezo utakuwa mgumu huku akikubali uwezo wa Geita kutokana na kiwango wanachoonyesha kwa sasa.
Pablo amesema wapinzani hao wana kikosi kizuri na wachezaji bora mmoja mmoja lakini sisi ni timu kubwa na tupo tayari kwa mtanange wa leo.
Pablo ameongeza kuwa bado hatujakata tamaa na mbio za ubingwa ndiyo maana tunajitahidi kutafuta alama tatu kwenye kila mchezo mpaka mwisho wa msimu.
“Tunajua mchezo utakuwa mgumu, Geita inacheza kitimu pia ina wachezaji wazuri mmoja mmoja, walitupa upinzani mkubwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Bado hatujakata tamaa na ubingwa ingawa tuna nafasi finyu lakini lengo letu ni kuhakikisha tunapata alama tatu katika kila mchezo kwa ajili ya heshima ya klabu na mashabiki,” amesema Pablo.
TUTAWAKOSA WAWILI LEO
Katika mchezo wa leo tutakosa huduma ya viungo wawili Jonas Mkude na Hassan Dilunga ambao ni majeruhi.
Mkude anaendelea vizuri na anatarajia kurejea uwanjani siku chache zijazo wakati Dilunga yupo nchini Afrika Kusini kwa matibabu.