Kocha Mkuu Pablo Franco, ameweka wazi kuwa bado hatujakata tamaa na ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa sababu tuna mechi nane zimebaki kabla ya kumaliza msimu.
Pablo amesema ingawa tupo nyuma kwa alama 10 dhidi ya vinara lakini kwa kuwa bado kuna idadi kubwa ya mechi zimebaki lolote linaweza kutokea na hatujakata tamaa.
Pablo ameongeza kuwa baada ya kutoka sare na Yanga katika mchezo wa Aprili, 30 tulijiweka katika mazingira magumu ya kutetea ubingwa lakini kutokana na ratiba kubana hata kwa wanaongoza lolote linaweza kutokea.
“Kama nilivyowahi kusema huko nyuma mbio za ubingwa bado zipo wazi. Tupo nyuma kwa pointi 10 lakini kama wanaongoza wataendelea kudondosha pointi nasi tukishinda zetu tunaweza kutetea ubingwa,” amesema Pablo.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Ruvu Shooting tuliobuka na ushindi wa mabao 4-1 Pablo amesema tumecheza vizuri na wachezaji walifuata maelekezo ingawa kipindi cha kwanza tulipoteza nafasi kadhaa za kufunga.
“Kwanza nimefurahi kwa ushindi huu mnono, mchezo ulikuwa mzuri tumetengeneza nafasi nyingi kipindi cha kwanza lakini hatukuzitumia vizuri. Tulivyorudi cha pili tulijirekebisha makosa na kufanikisha ushindi huu,” amesema Pablo.