Tupo kwa Mkapa Leo kuikabili Ruvu Shooting

Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku kuikabili Ruvu Shooting katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Kikosi kipo katika hali nzuri wachezaji wamefanya mazoezi ya mwisho jana hakuna aliyepata majeraha yatakayo mfanya kukosa mchezo wa leo.

Baada ya kukosa matokeo ya ushindi katika mechi tatu mfululizo kwa sasa tumejipanga kuhakikisha tunashinda leo ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuipambania ubingwa.

MATOLA AFUNGUKA

Kocha Msaidizi Seleman Matola, amesema mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora na nafasi mbaya waliyopo Ruvu hivyo tutaingia kwa kuchukua tahadhari zote.

Matola amesema haileti picha nzuri kwa timu kubwa kama Simba kucheza mechi tatu mfululizo bila kupata ushindi hivyo leo tutapambana kwa kila hali kupata pointi tatu.

“Ruvu haipo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo kwahiyo itapambana kuhakikisha inashinda, nasi tunalijua hilo na tupo tayari kuwakabili.

“Hatujapata ushindi katika mechi tatu za ligi na sio jambo zuri kwa timu kubwa kama Simba, tutahakikisha tunashinda leo ili kupunguza tofauti ya pointi dhidi yetu na wanaongoza,” amesema Matola.

TUMEWAFUNGA RUVU MARA MBILI MSIMU HUU

Kabla ya mechi ya leo tumekutana mara mbili na Ruvu Shooting msimu huu na tumeshinda mechi zote.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Novemba 19, 2021 tuliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Pia tulikutana na Ruvu katika mchezo wa Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Februari 16, tukaibuka na ushindi wa mabao 7-0.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER