Pablo: Hatuna Presha na mchezo wa kesho

Licha kuwa na tofauti kubwa ya pointi kati yetu na vinara wa ligi kuelekea mchezo wa kesho wa Derby dhidi ya Yanga, Kocha Mkuu Pablo Franco amesema kikosi chake hakina presha yoyote.

Pablo amesema tuna wachezaji bora kikosini ambao wamecheza mechi nyingi za aina hii kwa hiyo hakutakuwa na tofauti yoyote.

Pablo ameongeza kuwa ukiwa timu kubwa unafurahi kucheza mechi kubwa pia kama ya kesho hivyo tuko tayari kwa mapambano.

Akizungumzia mchezo huo Pablo amesema utakuwa mgumu lakini tumejiandaa kuhakikisha tunapata alama tatu ili kupunguza tofauti na kuwapa presha wanaoongoza.

“Hatuna presha yoyote kuelekea mchezo wa kesho. Simba ni timu kubwa na inapenda kucheza mechi kubwa pia. Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu lakini tumejipanga vizuri.

“Sisi tuko tayari, wachezaji wako kamili. Tunataka kuwapa furaha mashabiki wetu hasa baada ya kutupa sapoti baada ya kutolewa kwenye Michuano ya Shirikisho Afrika,” amesema Pablo.

Kwa upande wake mlinzi wa kulia Shomari Kapombe amesema baada ya malengo yetu ya kufuzu Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho kushindikana tumerejesha nguvu kwenye ligi na lengo ni kuwapa furaha Wanasimba katika mchezo wa kesho.

“Baada ya kutolewa Shirikisho Afrika sisi kama wachezaji tulikaa na kupanga kuhusu mchezo huu mkubwa ambao unavuta hisia kubwa, mashabiki wetu hawakujisikia vizuri na malengo ni kuwafurahisha kwa ushindi dhidi ya Yanga kesho,” amesema Kapombe.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER