Jeshi la Polisi limewatoa hofu mashabiki wanaotaka kuja uwanjani kesho kuisapoti timu katika mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Gandarmerie utakaopigwa saa nne usiku kuwa usalama utaimarishwa muda wote.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi Joseph Ngole amesema ulinzi utaimarishwa ndani na nje ya uwanja na maeneo ya karibu ili kila shabiki atakayehudhuria arudi salama nyumbani kwake.
Kamishna Ngole amesema kutakuwa na idadi kubwa ya polisi ndani na nje ya uwanja ambapo watakuwa wamevaa sare za polisi wengine wakiwa wapo kiraia ili kuhakikisha kila mtu anakaa salama.
Kamishna Ngole ameongeza kuwa pia kutakuwa na Polisi wa Usalama Barabarani (traffic) ambao watakuwa barabarani kwa ajili ya kusaidia kuondoa foleni wakati wa kwenda na kurudi uwanjani.
“Mashabiki mnaotaka kuja uwanjani kushangilia timu yenu njooni wala msiwe na hofu usalama umeimarishwa vya kutosha. Kutakuwa na idadi kubwa ya polisi ndani na nje ya uwanja.
“Pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nalo limeongeza mgambo zaidi ya 100 ambao watakuja kusaidia, kutakuwa pia na vikundi mbalimbali vya ulinzi shirikishi lengo ni moja kuhakikisha kila anayekuja uwanjani anarudi nyumbani salama,” amesema Kamishna Ngole.