Kikosi chetu leo kutashuka katika Uwanja wa Generali Mathieu Karekou uliopo mji wa Cotonou nchini Benin kuikabili ASEC Mimosas kwenye mchezo wetu wa tano wa Kombe la Shirikisho Afrika umbao utaanza saa moja usiku.
Tunaingia katika mchezo wa leo tukijua tupo ugenini hivyo tutachukua tahadhari zote lakini lengo letu la kwanza ni kuchukua pointi zote tatu.
ASEC haijapoteza mechi yoyote nyumbani lakini tumejipanga kuhakikisha tunavunja mwiko wao na kuwa timu ya kwanza kufanya hivyo.
PABLO AFUNGUKA
Kocha Mkuu Pablo Franco amesema tunahitaji kujihakikishia kutinga robo fainali ya michuano hii kwa kushinda mchezo wa leo ingawa haitakuwa kazi rahisi.
Pablo amekiri kuwa ASEC ni timu nzuri na inaweza kufanya chochote pia haijawahi kufungwa nyumbani lakini tumekuja kamili kuhakikisha tunavunja mwiko.
“Tumekuja kupambana kubadili historia yao ya kutofungwa nyumbani tunataka kuwa wa kwanza kuwafunga na kujihakikishia nafasi ya kutinga robo fainali,” amesema Pablo.
KIBU ATOA NENO
Mshambuliaji Kibu Denis amesema kwa upande wao wachezaji wapo tayari kuipigania timu na kuwapa furaha mashabiki lakini tutaingia kwa tahadhari kwakuwa ASEC ni timu bora.
“Haitakuwa mechi rahisi ASEC tuliwafunga nyumbani kwa hiyo watakuja kwa nia ya kulipa kisasi lakini tumejipanga kuwazuia, tutachukua tahadhari zote naamini tutapata ushindi kwa uwezo wa Mungu,” amesema Kibu.
HALI YA KIKOSI
Wachezaji wote 25 tuliosafiri nao wako fiti hakuna aliyepata majeraha na wamefanya mazoezi ya siku mbili hivyo benchi la ufundi litakuwa na wigo mpana wa kupanga kikosi.
HALI YA HEWA KAMA DAR
Hali ya hewa hapa katika Mji wa Cotonou haina tofauti na jijini Dar es Salaam ambayo ni joto hivyo wachezaji hawatapata changamoto kwa upande huo.
One Response