Tunarejea katika Ligi Kuu ya NBC

Baada ya ratiba ndefu ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi leo kikosi chetu kitacheza mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Biashara United utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku.

Takribani wiki mbili kikosi chetu kilikuwa nje ya nchi kwa ajili ya michuano hiyo na leo tunarejea tena kwenye ligi ya ndani lengo ni moja kuhakikisha tunakusanya alama tatu kwenye kila mchezo.

Mchezo wa leo ni wa kwanza wa mzunguko wa pili wa ligi na tumepanga kuhakikisha tunashinda kila mechi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutetea ubingwa.

KAULI YA KOCHA PABLO

Kocha Mkuu Pablo Franco, amesema mchezo utakuwa mgumu na tutaingia kwa kuiheshimu Biashara kutokana na ubora wao lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda.

Pablo amesema aliwatazama Biashara katika mechi ya FA na ile ya Ligi dhidi ya Namungo na kugundua wanacheza soka la pamoja kuanzia kwenye kuzuia hadi kushambulia.

Raia huyo wa Hispania ameongeza kuwa kuanzia leo tunapoanza mzunguko wa pili wa ligi tumejipanga kuhakikisha hatudondoshi alama yoyote.

“Mchezo utakuwa mgumu, Biashara ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri mmoja mmoja. Tunahitaji kushinda ili kupunguza idadi ya pointi iliyopo dhidi ya wanaongoza. Tunacheza katika Uwanja wa nyumbani na tunategemea kupata ushindi,” amesema Pablo.

MZAMIRU, BWALYA WAREJEA KUONGEZA NGUVU

Viungo Mzamiru Yassin na Rally Bwalya wamerejea kikosini baada ya kumaliza masuala yao ya kifamilia yaliyokuwa yakiwakabili.

Wawili hao walikosa mechi zetu za ugenini za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Gendarmerie na RS Berkane kutokana na sababu hizo.

TUTAWAKOSA NYOTA SITA

Katika mchezo wa leo tutawakosa wachezaji sita kutokana na kuwa  majeruhi. Nyota hao ni Chris Mugalu, Kibu Denis, Hassan Dilunga, Jonas Mkude, Aishi Manula na Sadio Kanoute.

Mugalu na Kibu ambao walikuwa nje ya uwanja kwa muda tayari wameanza mazoezi na utimamu wao wa mwili ukiwa sawa wataanza kushuka dimbani.

SHARE :
Facebook
Twitter

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER