Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Manispaa ya Berkane kuikabili RS Berkane katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi ambao utaanza saa nne usiku.
Mchezo wa leo utakuwa ni wa tatu katika michuano hii ambapo tumefanikiwa kukusanya alama nne katika mechi mbili na kuwa vinara wa Kundi D.
Pamoja na changamoto ya hali ya hewa ambapo nchini Morocco ni baridi kali wachezaji wetu wameendelea kuizoea na haitakuwa kikwazo kwenye mchezo wa leo.
PABLO AFUNGUKA
Kocha Mkuu Pablo Franco amesema tunafahamu mchezo utakuwa mgumu na wapinzani watahitaji kutumia nguvu kupata alama tatu lakini timu iko tayari kuwakabili.
Pablo amesema hatupaswi kuhofia chochote badala yake amewataka wachezaji kupambana muda wote ili kutetea nembo ya Simba kupata matokeo mazuri kwa kuwa kwa sasa sisi ni miongoni mwa timu kubwa Afrika.
Aidha, Pablo ameeleza kuwa tutawakosa baadhi ya wachezaji katika mchezo wa leo kutokana na majeruhi huku wengine wakiwa wagonjwa.
“Mara zote katika hatua hii mechi za ugenini zinakuwa ngumu. Kila timu inajitahidi kutumia vizuri uwanja wa nyumbani lakini sisi tuko tayari kupambana na hatuhofii chochote,” amesema Pablo.
MORRISON: TUKO TAYARI
Kiungo mshambuliaji Bernard Morrison, amesema wachezaji wote wako kwenye hali nzuri morali ipo juu na yeyote atakayepata nafasi atakuwa tayari kuiwakilisha timu.
“Sisi tupo tayari, tunajua tunachotakiwa kufanya. Tunajua haitakuwa mechi rahisi lakini tutahakikisha tunapamba kuisaidia timu,” amesema Morrison.
ERASTO NYONI ATOA NENO
“Tumejipanga kimwili na kiakili kuhakikisha tunashinda, haitakuwa mechi rahisi lakini tupo tayari. Tunahitaji sala na maombi ya Watanzania ili tufanikishe malengo yetu,” amesema Erasto.
One Response