Licha ya ushindi tuliopata dhidi ya Azam FC Kocha Mkuu Pablo Franco, amesema mchezo ulikuwa mgumu na ulitawaliwa na mbinu nyingi kutoka kila timu.
Amesema mechi ilikuwa nzuri ya kuvutia na tulitawala sehemu kubwa ingawa tulipoteza nafasi kadhaa ambazo zingetufanya kuibuka na ushindi mnono zaidi.
Pablo ameongeza kuwa ushindi tuliopata na kiwango tulichoonyesha umeongeza hali ya kujiamini kuelekea katika Michuno ya Mapinduzi itakayoanza wiki ijayo Visiwani Zanzibar.
“Mechi ilikuwa ngumu na ilitawaliwa na mbinu zaidi. Tulimiliki sehemu kubwa ya mchezo na tulipoteza nafasi za kufunga pamoja na penati,” amesema Pablo.
Kuhusu suala la kukosa penati tatu kutoka kwa wachezaji watatu tofauti Pablo amesema bado ana muda mfupi hivyo anaendelea kulifanyia kazi na kuwajengea nyota wetu hali ya kujiamini.
“Ni kweli kuna changamoto kwenye upigaji wa penati alianza kukosa Erasto Nyoni akafuata Bernard Morrison na leo Rally Bwalya. Bado nina muda mfupi kikosini tutaendelea kuwarekebisha hadi wakae sawa,” amesema Pablo.
One Response