Kocha Mkuu Pablo Franco, amewasifu wachezaji kwa kujituma muda wote wa mchezo na kutufanya kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Red Arrows ya Zambia.
Pablo amesema kila mchezaji alifanya kazi yake vizuri na kutimiza majukumu uwanjani jambo ambalo limemvutia katika mchezo wa leo.
Hata hivyo, Pablo amesema tulikuwa na uwezo kupata mabao zaidi ya matatu tuliyopata kama wachezaji wangeongeza umakini katika nafasi tulizotengeneza.
“Nafurahi kwa ushindi huu, lakini zaidi nimefurahi kwa jinsi wachezaji walivyocheza, wote wamejituma na wanafurahi kucheza mpira. Tulikuwa na nafasi ya kupata mabao manne hadi matano kipindi cha kwanza lakini tulipoteza umakini,” amesema Pablo.
Pablo ameongeza kuwa hali ya hewa haikuwa rafiki kutokana na uwanja kujaa maji yaliyosababisha mpira kukwama kwama na kupunguza ladha ya mchezo.
Akizungumzia mchezo wa marudiano utakaofanyika Desemba 5 nchini Zambia, Pablo ameweka wazi kuwa utakuwa mgumu lakini tuna muda wa wiki moja ya kujiandaa kabla ya kusafiri.
“Mechi hizi za mtoano mara nyingi huwa ngumu ugenini, tuna wiki moja ya kujiandaa kabla ya kurudiana, matumaini yetu ni kufanya vizuri na kufuzu hatua ya makundi,” amesema Pablo.
One Response